Baraza la Mawaziri la Japani laidhinisha mswada kudhibiti kampuni kubwa za teknolojia katika biashara ya simu janja

Baraza la Mawaziri la Japani limeidhinisha mswada ulioundwa kuzidhibiti kampuni kubwa za teknolojia ili kuhakikisha ushindani wa haki katika biashara ya simu janja.

Kampuni zinazoongoza za teknolojia ikiwa ni pamoja na Apple na Google zinadhibiti soko la teknolojia ya simu janja. Kumekuwa na wasiwasi kwamba utawala wao wa soko unaweza kutatiza maingizo mapya na kusababisha gharama kubwa kwa biashara zinazotumia huduma zao.

Mswada huo ulioidhinishwa jana Ijumaa utateua kampuni zitakazodhibitiwa katika maeneo manne: programu za uendeshaji, maduka ya programu, vivinjari vya intaneti na injini za intaneti za kutafuta taarifa.

Sheria iliyopendekezwa itafafanua mazoea ambayo yanazuia ushindani na yanahitaji kupigwa marufuku.

Kampuni zitakazoteuliwa zitapigwa marufuku kuzuia matumizi ya maduka ya programu na huduma za malipo ya kampuni shindani.

Pia zitapigwa marufuku kufanya miamala ya kibaguzi na washirika wa biashara.

Kampuni zitahitajika kuwasilisha ripoti ya kila mwaka juu ya utekelezaji wao wa sheria hiyo.

Wakiukaji watakabiliwa na faini ya asilimia 20 ya mauzo yao nchini Japani ikiwa ni mara tatu zaidi ya faini ya kuzuia biashara ya kampuni nyingine chini ya sheria iliyopo ya kukosa uaminifu. Kwa wahalifu wa kurudia, faini itaongezwa hadi asilimia 30.

Serikali inapanga kutaka kupitishwa kwa mswada huo wakati wa kikao cha sasa cha Bunge, kinachotarajiwa kuendelea hadi mwishoni mwa mwezi Juni.