Kim Jong Un ashuhudia majaribio ya urushaji wa makombora

Korea Kaskazini inasema kuwa Kiongozi Mkuu, Kim Jong Un, amesimamia zoezi la majaribio ya urushaji wa makombora yaliyotengenezwa na kampuni mpya ya jeshi la nchi hiyo.

Gazeti la Rodong Sinmun linalomilikiwa na Chama tawala cha Wafanyakazi limesema leo Ijumaa kuwa Kim alishuhudia majaribio ya urushaji wa makombora ya milimita 240 kutoka mtambo wa urushaji roketi nyingi, jana Alhamisi.

Gazeti hilo linasema kwamba makombora hayo yametengenezwa na kampuni mpya ya viwanda vya ulinzi wa taifa iliyoanzishwa chini ya Tume ya Pili ya Kiuchumi inayohusika na sekta ya utengenezaji silaha nchini humo.

Makala hiyo inaonyesha picha ya kombora likirushwa kutoka kwenye mtambo wa kuhamishika wa kurushia roketi.

Kim ameripotiwa kuyasifia makombora hayo na kusisitiza juu ya umuhimu wa kampuni hiyo ya viwanda vya ulinzi wa taifa kutekeleza mpango wa mwaka huu wa kutengeneza silaha kama ulivyopangwa.

Shirika la habari la Yonhap la Korea Kusini limewanukuu waangalizi wa mambo wakisema Korea Kaskazini inaonekana kuimarisha zaidi uendelezaji wa makombora yanayorushwa kwa roketi kama hatua ya kuyapeleka nchini Urusi kwa ajili ya kutumiwa na nchi hiyo kwenye uvamizi nchini Ukraine.

Jumatatu iliyopita, Korea Kaskazini ilifanya majaribio ya urushaji wa kile ilichokiita kuwa ni "makombora ya hali ya juu ya roketi" ambayo yanaaminika kuwa ni makombora ya balistiki ya masafa mafupi. Jeshi la Korea Kusini limesema kuwa Korea Kaskazini inataka kuonyesha uwezo wake na huenda ikatumai kuyauza kwa nchi zingine.