Urusi yaikosoa Marekani kwa kuipatia Ukraine makombora ya masafa marefu

Msemaji wa Rais wa Urusi Dmitry Peskov jana Alhamisi alisema kuwa Marekani imejihusisha moja kwa moja katika mgogoro kati ya Urusi na Ukraine kwa kuipatia silaha za masafa marefu, lakini hili halitabadilisha kimsingi matokeo ya “operesheni maalum ya kijeshi ya Urusi.”

Serikali ya Marekani juzi Jumatano ilifichua kuwa Mifumo ya Makombora ya Kimkakati ya Jeshi, ATACMS imewasili nchini Ukraine. Marekani ilituma silaha za masafa ya kati za aina hiyo mwaka jana. Vyombo vya habari vya Marekani vinaripoti kuwa makombora mapya yaliyosafirishwa hadi nchini Ukraine yana karibu mara mbili ya umbali wa kufanya mashambulizi wa hadi kilomita 300.

Bajeti ya hivi karibuni ya msaada wa kijeshi wa Marekani iliyotiwa saini na Rais Joe Biden juzi Jumatano inaruhusu utawala huo kutwaa mali za Urusi zilizoshikiliwa kwa vikwazo na kuzitumia kuisaidia Ukraine.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Ryabkov alikiambia chombo cha habari cha serikali kuwa kupunguza kiwango cha uhusiano wa kidiplomasia cha Urusi na Marekani ni chaguo moja ikiwa mali za Urusi zitatwaliwa.