Vyombo vya habari vya Israel: Matayarisho ya mashambulizi ya ardhini mjini Rafah yamekamilika

Chombo kimoja cha habari cha Israel kinaripoti kuwa vikosi vya nchi hiyo vimekamilisha matayarisho ya operesheni ya ardhini katika mji wa Rafah uliopo kusini mwa Gaza.

Watu wapatao milioni 1.2 wanajihifadhi mjini humo. Israel inajiandaa kuanzisha operesheni hiyo kama sehemu ya jitihada za kuliangamiza kabisa kundi la Hamas licha ya mashaka kutoka kwa mataifa mengine.

Chombo kikuu cha habari cha Israel cha Haaretz kiliripoti jana Alhamisi kuwa jeshi la Israel limeitaarifu serikali kuhusu ukamilishaji wa matayarisho yake. Vikosi vya Israel vilivyotumwa awali kaskazini na maeneo ya kati ya Ukanda wa Gaza vinasemekana kupelekwa kusini mwa ukanda huo. Ripoti hiyo ilisema tarehe ya operesheni hiyo itaamuliwa na serikali.

Jeshi la Israel liliendelea kutekeleza mashambulizi ya angani katika Ukanda wa Gaza jana Alhamisi. Mamlaka za afya katika ukanda huo zimesema watu 34,305 wameuawa hadi kufikia sasa.