Iran yaonyesha aina ya silaha zilizotumika kuishambulia Israel

Iran imewaonyesha wanahabari wa NHK kile inachodai kuwa ni aina ya silaha zilizotumika katika mashambulizi yake makubwa ya makombora na droni dhidi ya Israel mapema mwezi huu.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislam la Iran liliwaruhusu wanahabari hao kuingia kwenye kituo kimoja kilichopo kwenye viunga vya mji wa Tehran jana Alhamisi, ambapo makombora na droni zilizotengenezwa nchini humo zilionyeshwa.

Brigedia Jenerali Ali Balali, ambaye ni mkuu wa kituo hicho, alisema silaha zilizotumika katika mashambulizi hayo ni pamoja na makombora ya balistiki ya Emad, makombora yanayoongozwa ya Paveh, na droni zinazolipuka aina ya Shahed- 136.

Makombora ya Emad yana uwezo wa kuruka umbali wa kilomita 1,700 huku droni za Shahed-136 zikiripotiwa kuwa na uwezo wa kusafiri umbali wa kilomita zaidi ya 2,000.

Balali alisema kuwa Iran ilitumia mkakati wenye ukomo katika mashambulizi hayo na kuwa haikutumia makombora yake ya kisasa ili kuepuka hali ya msuguano kuongezeka zaidi. Aliongeza kuwa mkakati wa Iran ulilenga kuweka uzuiaji ili kuikatisha tamaa Israel isishambulie eneo lolote la Iran.