China yawatuma wanaanga watatu katika kituo cha anga za juu cha Tiangong

China imewatuma wanaanga watatu katika kituo chake cha anga za juu kinachoizunguka dunia kabla ya urushaji unaotarajiwa wa nchi hiyo wa chombo kisichokuwa na wanaanga mwezini.

Hatua hiyo ni ya hivi karibuni katika mashindano ya utafiti wa anga za juu dhidi ya Marekani.

Roketi inayosukuma chombo cha anga za juu cha Shenzhou-18 kikiwa na wanaanga hao kiliruka kutoka Kituo cha Urushaji wa Satelaiti cha Jiuquan kilichopo kaskazini magharibi mwa China jana Alhamisi.

Waananga hao watachukua nafasi ya timu ya wenzao ambao kwa sasa wapo katika kituo cha anga za juu cha Tiangong. Watatumia takribani miezi sita kufanya majaribio, kukarabati mitambo na kufanya shughuli zingine.

Vyombo vya habari vya China vinasema kuwa nchi hiyo itarusha chombo cha uchunguzi wa mwezi cha Chang'e-6 kisichokuwa na wanaanga mwezi ujao ikiwa ni mapema zaidi kutafiti upande wa mbali wa mwezi.

Marekani na India zinatafiti maeneo yaliyopo jirani na Ncha ya Kusini ya mwezi, ambako wanasayansi wanasema huenda kuna barafu. Barafu hiyo inaweza kubadilishwa kuwa maji ya kunywa na fueli.