Blinken athibitisha tena umuhimu wa uhusiano thabiti na China katika mkutano wa Shanghai

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken jana Alhamisi alikutana na Katibu wa Kamati ya Manispaa ya Shanghai ya Chama cha Kikomunisti cha China, Chen Jining mjini Shanghai.

Blinken alisema, "Tuna wajibu kwa watu wetu, na hakika, wajibu kwa dunia kusimamia uhusiano baina ya nchi zetu mbili kwa kuwajibika."

Chen alijibu kwa kusisitiza kuwa China na Marekani zinapaswa kuchagua ushirikiano badala ya makabiliano. Alisema uhusiano wa kidiplomasia baina ya China na Marekani ni uhusiano muhimu zaidi wa pande mbili duniani na uhusiano huo "umepiga hatua kuelekea mbele."

Blinken aliwasili katika uwanja wa ndege jijini Beijing baadaye siku hiyo. Amepangiwa kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi na huenda pia na Rais Xi Jinping leo Ijumaa. Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani alikutana na Rais Xi mwezi Juni mwaka jana.

Mikutano ya hivi karibuni inatarajiwa kugusia masuala ambayo Marekani na China zinatofautiana. Baadhi ya masuala hayo ni Taiwan, Bahari ya China Kusini na Ukraine.