Marekani yawasilisha makombora ya masafa marefu nchini Ukraine, yaahidi kutuma makombora zaidi

Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Ikulu ya Marekani Jake Sullivan juzi Jumatano aliwaambia wanahabari kuwa Marekani imewasilisha Mifumo ya Makombora ya Kimkakati ya Jeshi, ATACMS nchini Ukraine. Pia amesema Marekani itatuma makombora zaidi.

Utawala wa Marekani unasema msaada huo wa kijeshi wa kugharamia usafirishaji wa makombora ulipangwa kwa kupunguza matumizi katika bajeti yake ya sasa.

Waangalizi wa mambo wanasema nadharia sasa imeelekezwa kwa namna upatikanaji wa makombora ya masafa marefu kwa Ukraine utaathiri mgogoro huo.

Mwaka jana, Marekani ilitoa makombora ya masafa ya kati yenye umbali wa takriban kilomita 160. Vyombo vya habari vya Marekani viliripoti kuwa makombora hayo mapya yanaipatia Ukraine karibu mara mbili ya umbali wa kufanya mashambulizi wa hadi kilomita 300.

Taasisi ya Utafiti wa Vita ambayo ni jopo la ushauri la Marekani juzi Jumatano ilisema kuwa, “Kuwasili kwa makombora ya masafa marefu ya ATACMS katika viwango vinavyotosheleza kutaruhusu vikosi vya Ukraine kupunguza mipango ya usafirishaji ya Urusi na kutishia viwanja vya ndege vya Urusi katika maeneo ya nyuma kabisa.”