Maswali na Majibu: Maambukizi ya kupe (3)

SFTS (3)

NHK inajibu maswali yanayohusiana na kuhakikisha usalama kwenye maisha yetu ya kila siku. Magongwa yanayoenezwa na kupe wanaoishi kwenye maeneo ya misitu na mashamba yamekuwa yakiongezeka katika miaka ya hivi karibuni. Magonjwa haya yanaweza kusababisha dalili kama vile homa ama kuharisha na huenda yakasababisha kifo kwenye baadhi ya visa. Mfululizo huu unajadili masuala ya kuzingatia, na njia ya kuzuia kung’atwa na kupe. Katika kipengele hiki cha tatu, tunaangazia magonjwa ambukizi yanayoenezwa na kupe.

Kuna magonjwa anuai yanayoenezwa na kupe, lakini miongoni mwa magonjwa hayo ni, SFTS, ama homa kali ya ugonjwa wa thrombocytopenia, unaozua wasiwasi mkubwa. Wagonjwa wanaoumwa huonyesha dalili kama homa, kukohoa, kutapika na kuharisha. Katika visa vikali zaidi, unaweza kusababisha kuvuja damu kusikokoma, hadi kusababisha kifo. Hakuna matibabu yenye ufanisi kwa ugonjwa huo na kiwango cha vifo kinaaminika kuwa kati ya asilimia 10 hadi 30. Taasisi ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi inasema kwamba mnamo mwaka 2023, visa 133 viliripotiwa, ikiwa ni idadi ya juu kabisa katika kipindi cha miaka 11 ambacho ulinganishaji wa data ulianza kupatikana. SFTS inaambukizwa kupitia kung’atwa na kupe, lakini kuna visa ambapo maambukizi hutokea kupitia wanyama pendwa walioambukizwa. Mwezi Julai mwaka jana, maambukizi baina ya wanadamu yaliripotiwa kwa mara ya kwanza nchini Japani.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia April 25, 2024.