Sarafu ya yeni yashuka thamani hadi kiwango cha juu cha 155 dhidi ya dola

Sarafu ya yeni ya Japani inaendelea kushuka thamani dhidi ya dola ya Marekani, ikifikia kiwango cha juu cha yeni 155 katika soko la kubadilishia fedha za kigeni la Tokyo leo Alhamisi. Wawekezaji wanafuatilia kwa karibu sarafu hizo mbili wakati Benki Kuu ya Japani, BOJ ikianza mkutano wake wa sera wa siku mbili hadi kesho Ijumaa.

Yeni haijawahi kuwa katika kiwango cha 155 dhidi ya dola tangu mwaka 1990. Wafanyabiashara wamekuwa wakiiuza yeni na kununua dola kutokana na uchumi imara wa Marekani. Pia wanatoa sababu ya mtazamo kuwa Benki Kuu ya Marekani itachelewesha kupunguza kiwango cha riba.

Kadhalika wawekezaji wanakisia kwamba BOJ haitaongeza viwango vya riba hivi karibuni.

Waangalizi wa masoko wanaamini tofauti ya kiwango cha riba iliyopo kati ya Marekani na Japani huenda ikaendelea, na kusababisha faida kubwa katika dola.

Waziri wa Fedha wa Japani Suzuki Shunichi aliulizwa kuhusu yeni inayoshuka thamani leo Alhamisi kwenye mkutano wa kamati ya Baraza la Juu la Bunge. Amesema serikali inafuatilia soko hilo kwa karibu na dhamira yake ya kuchukua hatua stahiki inayojikita katika ufuatiliaji wake haijabadilika.

Suzuki ameongeza kuwa hawezi kuzungumzia zaidi suala hilo wakati huu.