Urusi yapiga kura ya turufu dhidi ya rasimu ya azimio la UN la kuzuia mashindano ya silaha za nyuklia angani

Urusi imepiga kura ya turufu dhidi ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, linalofadhiliwa na Japani na Marekani ambalo linalenga kuzuia mashindano ya silaha za nyuklia angani.

Rasimu ya azimio hilo inataka kufuata kikamilifu Mkataba wa Anga ya Juu, ambao unakuza matumizi ya amani ya anga.

Pia inataka kupiga marufuku uendelezaji wa nyuklia na silaha zingine za maangamizi ya halaiki kwa ajili ya kupelekwa kwenye mzingo wa dunia.

Katika kura za jana Jumatano, wanachama 13 kati ya 15 wa baraza hilo waliunga mkono rasimu ya azimio hilo, lakini China ilijizuia kupiga kura na Urusi ikatumia kura yake ya turufu.

Balozi wa Marekani katika UN, Linda Thomas-Greenfield alisema baada ya kura hiyo: "Hii si mara ya kwanza kwa Urusi kudhoofisha utaratibu wa kimataifa wa kuzuia ueneaji wa silaha za nyuklia."

Balozi wa Japani katika UN, Yamazaki Kazuyuki alisema ni vigumu kuelewa kwa nini baraza hilo haliwezi kuwa na umoja katika ahadi rahisi lakini muhimu.

Balozi wa Urusi katika UN, Vassily Nebenzia alisema suala hilo linapaswa kujadiliwa na wanachama wote wa UN na sio Baraza la Usalama pekee.

Alielezea rasimu ya azimio hilo kama propaganda za kisiasa, akisema kwamba "lengo pekee la Marekani kuwasilisha rasimu hii ilikuwa ni kuikashifu Urusi."