TikTok yaapa kupinga sheria mpya inayoweza kupiga marufuku app yake ya kushirikisha video

Mkurugenzi Mtendaji wa TikTok, Zi Chew anasema kampuni hiyo itapinga mahakamani mswada uliotiwa saini na Rais wa Marekani Joe Biden kuwa sheria ambayo inaweza kupiga marufuku app maarufu ya kushirikisha video nchini humo ya TikTok.

Bunge la Seneti la Marekani lilipitisha mswada huo juzi Jumanne na Biden aliutia saini jana Jumatano. TikTok itapigwa marufuku ikiwa mwendeshaji wa China ByteDance hataiuza ndani ya siku 270. Biden anaweza kuongeza tarehe ya mwisho kwa hadi siku 90.

Katika ujumbe wa video, Chew alisema, "Usifanye makosa, hii ni marufuku kwa TikTok na marufuku kwako na sauti yako. Tuna imani kwamba tutaendelea kupigania haki yako katika mahakama. Ukweli na Katiba iko upande wetu na tunatarajia kushinda tena.”

App hiyo inasemekana kuwa na watumiaji milioni 170 nchini Marekani.

Kumekuwa na wasiwasi unaoongezeka kuwa app hiyo inaweza kuhatarisha usalama kwani serikali ya China inaweza kuitumia vibaya kupata taarifa. Lakini wengine wanapinga marufuku hiyo, wakisema kuwa inakiuka haki ya uhuru wa kujieleza.