Waziri wa Ulinzi wa Urusi adhamiria kuongeza mashambulizi dhidi ya silaha za Magharibi

Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu amesema vikosi vyake vitafanya mashambulizi zaidi nchini Ukraine dhidi ya vituo vya usafirishaji na kambi za kuhifadhi silaha zinazotolewa na Marekani na nchi za Bara la Ulaya.

Katika mkutano uliofanyika jana Jumanne, Shoigu alisema, “Utawala wa Ukraine haukuweza kufanikisha lengo lake katika mashambulizi ya kujibu yaliyoandaliwa na wakufunzi wa NATO. Maafisa wetu wa kijeshi wameondoa dhana ya ubora wa silaha za nchi za Magharibi.”

Shoigu aliongeza kuwa wanajeshi wa Urusi waliopo mistari ya mbele vitani tayari wameshika hatamu, na atawaongezea nguvu na kutengeneza silaha na vifaa zaidi.

Viongozi wa Ukraine wameshuhudia ongezeko la mashambulizi ya mara kwa mara kwenye mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa Kharkiv. Rais Volodymyr Zelenskyy alisema shambulizi moja kwenye mnara wa televisheni ni sehemu ya juhudi ya kulifanya eneo hilo kutokalika.