Maseneta wa Marekani wapitisha mswada unaotoa matumaini kwa msaada kwa Ukraine

Bunge la Seneti la Marekani lilipitisha mswada wa bajeti ya dharura ikijumuisha msaada wa ziada kwa jeshi la Ukraine. Mswada huo unatarajiwa kuwa sheria baada ya Rais Joe Biden kuutia saini.

Wiki iliyopita, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walimaliza miezi kadhaa ya mabishano na kupitisha bajeti hiyo. Rais Joe Biden tayari ameahidi kutia saini kuwa sheria.

Mswada huo kwa Ukraine, unajumuisha msaada wa zaidi ya dola bilioni 60. Utawawezesha maafisa katika Wizara ya Ulinzi ya Marekani kusafirisha vifaa vya kijeshi ndani ya siku kadhaa. Pia utaruhusu mamlaka za Marekani kutaifisha mali za Urusi zilizozuiliwa na kuzihamisha ili kuifadhili Ukraine kurejea katika hali ya kawaida.

Bajeti hiyo imetenga zaidi ya dola bilioni 26 kusaidia juhudi za Israel za kujilinda dhidi ya Iran na mawakala wake. Pia itatoa dola bilioni 8 kwa juhudi huko Taiwan na eneo la Indo-Pasifiki ili "kukabiliana" na China.