Japani yaanza operesheni ya tahadhari maalum dhidi ya ugonjwa wa kuzirai kutokana na joto kali

Serikali ya Japani imeanza operesheni yake ya kila mwaka ya mfumo wake wa tahadhari ya kuzuia magonjwa yanayohusiana na joto. Mfumo huo unajumuisha Tahadhari mpya Maalum dhidi ya Ugonjwa wa Kuzirai kutokana na Joto Kali.

Wizara ya Mazingira na Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Japani vimeanzisha mfumo huo leo Jumatano.

Tahadhari hiyo itatolewa kwa mikoa ambapo kipimo cha joto kinachotokana na vipengele kama vile halijoto na unyevunyevu, kinatarajiwa kufikia nyuzi 35 au zaidi katika maeneo yote yanayopimwa.

Ni kiwango kimoja juu cha tahadhari dhidi ya kile cha kawaida cha ugonjwa huo, ambayo hutolewa wakati kipimo hicho kinapofikia nyuzi 33 au zaidi.

Tahadhari hiyo mpya inatarajiwa kuonyesha viwango vya juu vya halijoto ambavyo vinaweza kuleta hatari kubwa kiafya kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika eneo pana.

Mikoa ambapo tahadhari itatolewa itatakiwa kuchukua hatua madhubuti za kuzuia ugonjwa wa kuzirai kutokana na joto kali.

Serikali za kimaeneo lazima zitenge mapema maeneo ya umma na binafsi yenye viyoyozi kama “makazi ya muda ya kupoza mwili” na kuyafungua tahadhari itakapotolewa.