Maswali na Majibu: Maambukizi ya kupe (1)

(1) Biolojia ya kupe

NHK inajibu maswali kuhusiana na kuhakikisha usalama katika maisha ya kila siku. Magonjwa yanayoambukizwa na kupe wanaoishi katika maeneo ya msitu na mashamba yamekuwa yakiongezeka katika miaka ya hivi karibuni. Wakati unapoambukizwa, dalili huenda zikajumuisha homa au kuharisha ambazo zinaweza zikasababisha kifo hali ikiwa mbaya zaidi. Mfululizo huu unajadili tahadhari unazopaswa kuchukua na hatua za uzuiaji. Katika sehemu hii ya kwanza, tunaangazia biolojia ya kupe.

Kupe huwa hatari kuanzia msimu wa chipukizi hadi pukutizi. Kwa sababu watu wengi hufurahia kuchuma mbogamboga za mwituni au kwenda matembezi milimani wakati wa msimu huu, hatari ya kuumwa inaongezeka. Mtafiti aliyebobea katika biolojia ya kupe anasema kwa kawaida wao hujificha upande wa chini wa majani wakisubiri wanyama kupita.

Siku zilizopita, kupe walijulikana kuuma wanyama wa mwituni katika milima kama vile nguruwe mwitu na mbawala, lakini katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na visa vinavyoongezeka vya kupe kunyonya damu ya mbwa au paka pendwa na pia binadamu. Mtafiti huyo anaonya kuwa kupe wanapanua makazi yao kwani wanyama wa mwituni wanaonekana katika maeneo ya makazi mara kwa mara kuliko awali.

Taarifa hii ni sahihi kufikia Aprili 23, 2024.