Maafisa waandamizi wa UN watoa onyo juu ya sheria ya uhamiaji ya Uingereza

Maafisa wawili waandamizi wa Umoja wa Mataifa, UN wametoa onyo juu ya sheria ya Uingereza ya kuwapeleka nchini Rwanda baadhi ya wanaotafuta hifadhi, wakisema itakuwa na athari mbaya kwa haki za binadamu na ulinzi wa wakimbizi.

Kamishna Mkuu wa UN wa Kuhudumia Wakimbizi Filippo Grandi na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN, Volker Turk walitoa onyo hilo katika taarifa ya pamoja jana Jumanne.

Hatua hiyo inakuja baada ya bunge la Uingereza kupitisha mswada wa kuwapeleka Rwanda baadhi ya wahamiaji ambao waliingia nchini Uingereza, katikati ya upinzani mkali kutoka kwa makundi ya kutetea haki za binadamu.

Grandi alisema katika taarifa, “Sheria hii mpya inaashiria hatua zaidi mbali na utamaduni wa Uingereza wa muda mrefu wa kutoa hifadhi kwa wale wenye mahitaji, kinyume na Mkataba wa Wakimbizi.”

Alitoa wito kwa serikali ya Uingereza kufikiria upya mpango wake wa kuhamisha wanaotafuta hifadhi, akisema, "Mpango huu unalenga kuhamisha jukumu la ulinzi kwa wakimbizi, kudhoofisha ushirikiano wa kimataifa na kuweka mfano wa kimataifa unaotia wasiwasi."

Turk alisema, “Ni muhimu katika kulinda haki za binadamu na utu wa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta ulinzi kwamba kuondolewa kwao wote kutoka Uingereza kunafanywa baada ya kutathmini hali zao maalum za kibinafsi kwa kufuata kikamilifu haki za binadamu za kimataifa na sheria ya wakimbizi."

Juzi Jumatatu Waandishi Watatu Maalum wa UN pia walitoa taarifa juu ya mswada huo.

Walisema, “mashirika ya ndege na waendeshaji wa usafiri wa anga wanaweza kujihusisha katika ukiukaji wa haki za binadamu za kimataifa na maagizo ya mahakama kwa kuwezesha kuwaondoa wahamiaji hao kuwapeleka nchini Rwanda.”

Walisema, “Ikiwa mashirika ya ndege na mamlaka za anga zitatekeleza maamuzi ya taifa ambayo yanakiuka haki za binadamu, lazima wawajibike kwa vitendo vyao.”