Japani kuanzisha vituo vya mafunzo kufanikisha huduma ya afya kwa wote

Serikali ya Japani inapanga kufungua kituo cha mafunzo kwa maafisa wa umma wa afya wa kigeni ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufanikisha huduma za afya kwa wote, au UHC.

UHC inalenga kuhakikisha kila mtu anapata huduma bora ya afya na huduma za matibabu bila kumsababishia changamoto za kifedha.

Mpango huo wa kufungua kituo nchini Japani mwaka ujao kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani na Benki ya Dunia unakuja baada ya mada hiyo kujadiliwa kwenye mkutano wa viongozi wakuu wa Kundi la Nchi Saba zilizostawi zaidi kiviwanda, G7 mnamo Mei mwaka jana.

Viongozi wa G7 waliweka wazi kwenye taarifa yao ya pamoja dhamira yao ya kufanya kazi kwa pamoja ili kufanikisha UHC kufikia 2030.

Wizara ya Afya, Kazi na Ustawi wa Jamii ya Japani ilisema kituo hicho kitawakaribisha maafisa wa afya na fedha kutoka mataifa ya Afrika na Kusini Mashariki mwa Asia na kwingineko.

Wizara hiyo iliongezea kuwa, programu za mafunzo zitajikita kwenye kujifunza mfumo wa afya kwa wote wa Japani na huduma za uuguzi, pamoja na jinsi ya kufadhili miradi kama hiyo.