Kiongozi Mkuu wa Iran hajarejea uwezekano wa kulipiza kisasi wa Israel

Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, amepongeza shambulio la hivi karibuni la nchi hiyo dhidi ya Israel pasipo kurejea uwezekano wa shambulio la kulipiza kisasi la Israel.

Iran ilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya Israel kuanzia Aprili 13. Ijumaa iliyopita, mlipuko ulitokea katikati mwa Iran. Vyombo kadhaa vya habari vya Marekani viliripoti kwamba lilikuwa shambulio la kulipiza kisasi la Israel.

Kituo cha televisheni kinachoendeshwa na serikali ya Iran kimeripoti kwamba Khamenei alizungumza na makamanda wa vikosi vya kijeshi vya nchi hiyo jana Jumapili. Kwenye hotuba yake, alirejea shambulio la Iran. Alisema upande mwingine wanajali kuhusu makombora mangapi walirusha ama kufikia shabaha zao, lakini ni muhimu kwamba watu wa Iran na jeshi wameonyesha nia yao thabiti kwa dunia.

Hakugusia hatua za hivi karibuni za Israel zinazoonekana za kulipiza kisasi.

Waangalizi wa mambo wanasema kiongozi huyo mkuu wa Iran aliashiria kuwa nchi hiyo kwa sasa haina nia ya kuongeza hali ya wasiwasi kwa kufanya mashambulio zaidi.

Juzi Jumamosi, mlipuko mwingine ambao haukujulikana chanzo chake uliripotiwa kutokea katika kambi ya kundi la wanamgambo nchini Iraq linaloungwa mkono na Iran.