Urusi yaongeza hatua za ulinzi mwezi mmoja baada ya shambulio kwenye ukumbi wa tamasha

Leo Jumatatu unatimia mwezi mmoja tangu kutokea kwa shambulio la kigaidi lililosababisha vifo katika ukumbi mmoja wa tamasha jirani na Moscow. Serikali ya Urusi imeripotiwa kuongeza hatua za kiulinzi, na kwamba inaonekana zinajumuisha kuwabana zaidi wahamiaji wasiokuwa na vibali.

Watu zaidi ya 140 walifariki katika tukio hilo lililotokea Machi 22. Lilikuwa shambulio la kigaidi lililosababisha maafa makubwa kuwahi kutokea Urusi katika kipindi cha miongo miwili.

Kundi la Islamic State linaaminika kuhusika na shambulio hilo. Raia wanne wa Tajikistan wameshtakiwa kwa kutekeleza shambulio hilo.

Utafiti uliofanywa nchini Urusi unaonyesha kwamba idadi inayoongezeka ya watu wanajihisi kutishiwa na ugaidi.

Watu wengi katikati mwa Moscow wameiambia timu ya NHK kwamba mamlaka zinapaswa kuimarisha hatua kwa wahamiaji kutoka katikati mwa Asia.

Wizara ya mambo ya ndani mapema mwezi huu ilisema imefanya msako dhidi ya wahamiaji wasio na vibali katika maeneo zaidi ya 10,000 yakiwemo maeneo ya ujenzi jijini Moscow.

Rais Vladmir Putin ameshinda kwa kishindo uchaguzi wa urais uliofanyika Machi, na ataanza muhula wake wa tano kama rais Mei 7. Anaonekana kuimarisha hatua za ulinzi kwa sababu mashambulio ya kigaidi yanaweza kuyumbisha utawala wake.