Baraza la Wawakilishi la Marekani lapitisha msaada kwa Israel

Baraza la Wawakilishi la Marekani limepitisha mswada wa kuipatia Israel msaada wa dharura wenye thamani ya dola bilioni 26.3.

Mswada huo ulipitishwa kwa kupata uungwaji mkono mkubwa wa vyama vyote viwili ambapo kura 366 ziliunga mkono na 58 zilipinga juzi Jumamosi. Baraza hilo awali liliidhinisha nyongeza ya msaada wa kijeshi kwa Ukraine.

Fedha hizo zitaripotiwa kutumika kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa anga wa Israel na kupanua uwezo wa kuzalisha silaha, pamoja na msaada wa kibinadamu.

Mara tu baada ya mswada huo kupitishwa na Bunge la Seneti, Rais Joe Biden atausaini kuwa sheria.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin anasema sheria hiyo itairuhusu wizara yake kusaidia ulinzi wa Israel dhidi ya Iran na mawakala wake.

Iran ilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya Israel mnamo Aprili 13 na 14. Jeshi la Israel lilisema liliyazuia mashambulizi mengi kati ya hayo.

Kundi la wapiganaji wa Kishia la Hezbollah lenye makazi yake nchini Lebanon, pia liliishambulia Israel.

Wabunge wa Marekani wamekuwa wakitoa wito wa kutolewa msaada wa haraka kwa Israel huku kukiwa na ukosoaji juu ya kuongezeka kwa idadi ya vifo vya raia kwenye Ukanda wa Gaza.