NYT: Shambulizi la Israel laharibu mfumo wa ulinzi wa anga wa Iranan

Gazeti la The New York Times la nchini Marekani limesema mlipuko uliotokea karibu na kambi ya anga nchini Iran juzi Ijumaa uliharibu mfumo wa ulinzi wa anga ambao unalinda eneo lenye vituo vya nyuklia.

Gazeti hilo kubwa nchini humo liliwanukuu maafisa wa nchi za Magharibi na wa Iran ambao walisema kwamba silaha ya Israel iliyotumika katika shambulizi la kulipiza kisasi dhidi ya Iran iliharibu mfumo wa ulinzi unaohusika kubaini na kuharibu vitisho vya angani karibu na Natanz katika jimbo la Isfahan lililopo katikati mwa nchi hiyo.

Ripoti hiyo iliwanukuu maafisa wa nchi za Magharibi wakisema shambulizi hilo “lilifanyika ili kutuma ujumbe kwa Iran kwamba Israel inaweza kukwepa mifumo ya ulinzi ya Iran bila kugundulika na kuiharibu.”

Vyombo vya habari vya Iran juzi Ijumaa viliripoti kuwa kulikuwa na mlipuko karibu na kambi ya anga ya Isfahan na kwamba droni kadhaa ndogo zilidunguliwa.

Israel na Iran zinaendelea kufanyiana mashambulizi ya kulipiza kisasi. Hata hivyo, pande zote mbili ni dhahiri zinajaribu kuepuka kuongeza hali hiyo na kuwa vita kubwa.

Waangalizi wa mambo wanasema kwamba Israel ilitumia shambulizi la juzi Ijumaa ili kuifuatilia Iran kwa kuonesha uwezo wake mkubwa wa kijeshi.

Katika hatua nyingine, kundi la wanamgambo wa Kiislam wa Shia linaloungwa mkono na Iran linalofahamika kama Popular Mobilization Forces lililopo nchini Iraq jana Jumamosi lilisema kwenye mtandao wa kijamii kuwa mlipuko ulitokea katika kambi yake takribani kilomita 50 kusini mwa mji mkuu wa Baghdad.

Shirika la habari la Reuters lilimnukuu mfanyakazi wa hospitali akisema mtu mmoja aliuawa na wengine sita kujeruhiwa.

Wasiwasi unazidi kuongezeka juu ya kuvurugika kwa hali katika eneo la Mashariki ya Kati.