China yafanya maonesho ya meli zake za kivita kabla ya mkutano wa vikosi vya wanamaji

China imeonesha baadhi ya meli zake za kivita kwa vyombo vya habari vya kigeni kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitano, kabla ya mkutano wa kimataifa unaowajumuisha pamoja maafisa wa ngazi za juu kutoka nchi 29.

Jeshi la wanamaji la China liliwaruhusu waandishi wa habari wa kigeni kutazama meli nne za kivita, zikiwemo meli za kudungua makombora pamoja na meli inayotumika katika shughuli za ugavi na mahitaji, katika mji wa bandari wa mashariki wa Qingdao, ambako ndiko makao makuu ya Kikosi cha Meli za Kivita cha Bahari ya Kaskazini cha China.

Jeshi hilo la wanamaji ni mwenyeji wa Kongamano la 19 la Vikosi vya Wanamaji wa Pasifiki ya Magharibi huko Qingdao kuanzia leo Jumapili. Afisa wa juu kabisa kutoka Kikosi cha Kujihami cha Majini cha Japani ni miongoni mwa washiriki.

Maafisa hao wa jeshi wanatarajiwa kubadilishana mawazo kuhusu kanuni zinazoangazia uwezekano wa ajali baharini.

Mikutano baina ya nchi mbili pia inatarajiwa kufanywa kando ya mkutano huo.

Jana Jumamosi, msemaji wa jeshi la wanamaji la China aliwaambia waandishi wa habari kwamba China iko tayari kuzingatia ushirikiano wa pande nyingi na pia kukabiliana kwa pamoja juu ya hatari zinazohusu usalama wa baharini.

Nchi nyingi zinazidi kuwa na wasiwasi na shughuli za baharini za China katika Bahari ya China Kusini na Mashariki. Waangalizi wa mambo wanasema China huwa na nia ya kuzifuatilia nchi hizo kwa kuonesha uhodari wa vikosi vyake vya majini, huku ikisisitiza kujitolea kwake katika ushirikiano wa kimataifa.