Wananchi wa Shanghai wawatia moyo watu walioathirika na tetemeko la ardhi la katikati mwa Japani

Watu katika mji wa Shanghai wanaandika jumbe kuwatia moyo watu wa mkoa wa Ishikawa uliopo katikati mwa Japani ambao uliharibiwa vibaya na tetemeko la ardhi lililotokea Siku ya Mwaka Mpya.

Tomioka Hitomi ambaye anatoka mkoa wa Ishikawa na anaishi Shanghai anafanya maonesho kuhusiana na madhara ya tetemeko hilo la ardhi katika duka la kufanya manunuzi katika mji huo. Tukio hilo ambalo lilianza juzi Ijumaa na litadumu hadi Mei 5, liliandaliwa kwa ushirikiano na wafanyakazi wa serikali ya Ishikawa.

Maonesho hayo yanajumisha picha za mandhari ya mkoa huo iliyoharibika, ikiwa ni pamoja na maeneo ya makazi ya Mji wa Suzu na uwanja wa besiboli uliopo katika Mji wa Noto ambao ulipigwa na tsunami.

Bidhaa kutoka mkoa huo pia zinauzwa. Bidhaa hizo ni pamoja na pombe ya kitamaduni ya Kijapani ya sake na urembo wa lakari “urushi.”

Wanunuaji wapo huru kuandika jumbe kwa ajili ya watu wa Ishikawa. Baadhi yao waliandika kuwatakia kurejea mapema katika hali ya kawaida na wengine waliandika maneno ya kuwatia moyo na kuwaonea huruma kwa kutumia lugha ya Kijapani ama Kichina.

Waratibu wa maonesho hayo wanapanga kutuma jumbe hizo mapema mwezi wa Mei kwa vikundi vya misaada vinavyosaidia maeneo yaliyoathiriwa

Mwanamke mmoja raia wa China mwenye umri wa miaka ya 40 ambaye alisafiri hadi Ishikawa miaka minne iliyopita alielezea uungaji mkono wake kutoka Shanghai.

Tomioka alisema ndugu zake waliopo Mji wa Wajima bado wamehama makazi yao. Alisema kwamba jumbe nyingi kutoka kwa watu wa China zitawatia moyo kwa kiasi kikubwa watu wa Ishikawa.