Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa kuzuru Nagasaki

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, UN Linda Thomas-Greenfield yupo ziarani katika nchi za Korea Kusini na Japani kama sehemu ya juhudi za kudhibiti mipango ya nyuklia na makombora ya Korea Kaskazini. Balozi huyo atatembelea Nagasaki ambao ni moja kati ya miji miwili iliyowahi kushambuliwa kwa mabomu ya atomiki.

Thomas-Greenfield alizungumza na NHK jijini Tokyo jana Alhamisi kabla ya ziara hiyo.

Alisema, "Wajumbe wengi huzuru mji wa Hiroshima, na watu wa Nagasaki pia wamekuwa na tajiriba sawia. Na nilitaka kuangazia tajiriba ya Nagasaki, na kuzungumza na watu huko."

Ziara ya Thomas-Greenfield mjini humo, ambayo ni ya kwanza kufanywa na Balozi wa Marekani katika UN, itafanyika kabla ya yeye kuondoka nchini Japani kesho Jumamosi. Anatarajiwa kukutana na maafisa wa eneo hilo na kuzungumza na wanafunzi.

Balozi huyo alitumia siku kadhaa nchini Korea Kusini kama sehemu ya ziara yake ya kuangazia matishio kutoka kwa Korea Kaskazini. Ziara hiyo inafuatia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika mwezi uliopita, ambapo Urusi ilitumia kura yake ya turufu kupinga azimio lililolenga kuongeza muda wa mamlaka ya jopo la wataalamu wanaofuatilia vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini.

Thomas-Greenfield alisema, "Tutafanya kazi ndani ya UN, pamoja na washirika wetu wa Japani, Korea Kusini, na pia wengine, kutafuta njia zingine za kupata uchambuzi na ripoti tunazohitaji ili kuhakikisha kwamba vikwazo hivyo vinatekelezwa."