Marekani na Uingereza zawawekea vikwazo raia na kampuni za Iran kufuatia shambulizi kubwa nchini Israel

Marekani na Uingereza zimetangaza vikwazo dhidi ya raia na kampuni za Iran kufuatia shambulizi kubwa la kombora na droni lililotekelezwa na Iran nchini Israel mwishoni mwa juma lililopita.

Serikali ya Marekani ilisema katika taarifa jana Alhamisi kuwa inawalenga watu 16 na kampuni mbili zilizowezesha utengenezaji wa droni za Iran. Mali na maslahi yao nchini Marekani zinashikiliwa chini ya vikwazo hivyo.

Kwa upande wa Uingereza pia ilitangaza vikwazo jana Alhamisi dhidi ya watu saba na kampuni sita ambazo ilisema zimewezesha shughuli za Iran za kudhoofisha uthabiti Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na shambulizi lake la moja kwa moja dhidi ya Israel.

Wanaolengwa ni pamoja na Kikosi cha Wanamaji cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na watendaji wakuu wa kampuni ya Iran. Mali za watu na kampuni zilizolengwa zitashikiliwa.