IRGC: Maeneo ya nyuklia ya Israel yatalengwa ikiwa vituo vya nyuklia vya Iran vitashambuliwa

Kamanda mwandamizi wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, IRGC ameonya kuwa vituo vya nyuklia vya Israel vitalengwa ikiwa nchi hiyo itachukua hatua dhidi ya maeneo ya nyuklia ya Iran.

Chombo cha habari cha Tasnim, ambacho kina uhusiano na IRGC, kilitoa maoni ya Brigedia Jenerali Ahmad Haqtalab jana Alhamisi.

Alizungumza wakati kukiwa na mashaka kuwa Israel inaweza ikashambulia maeneo ya nyuklia ya Iran katika kulipiza kisasi shambulizi la kombora na droni lililotekelezwa na Iran dhidi ya Israel mwishoni mwa wiki iliyopita.

Haqtalab, ambaye amekabidhiwa jukumu la kuhakikisha usalama wa maeneo ya nyuklia ya Iran, alisema vituo vya nyuklia vya Israel vimetambuliwa.

Aliongeza kuwa ikiwa Israel itajaribu kutumia tishio la kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran ili kuishinikiza, kanuni ya nyuklia ya nchi yake huenda ikapitiwa upya.

Iran kwa sasa inadumisha kuwa mpango wake wa nyuklia ni kwa ajili ya madhumuni ya amani na kwamba haina nia ya kumiliki silaha za nyuklia.

Serikali ya Israel imekuwa ikijadili mwitikio wake kwa shambulizi la Iran. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema wakati wa mkutano wa Baraza la Mawaziri juzi Jumatano kuwa “taifa la Israel litafanya kila kinachohitajika kujilinda.”