Taarifa

Uelewa Juu ya Kimbunga

1. Hatari zinazotokea baada ya kimbunga kupita.
2. Madhara yanayotokana na pepo kali.
3. Hatari za maji mengi ya baharini yanayosababishwa na kimbunga.
4. Kufurika kwa mito.
1. Hatari zinazotokea baada ya kimbunga kupita.

Bila shaka ni hatari kuwa nje pale kimbunga kinapokaribia, pia ni hatari kutembea ama kuendesha gari baada ya hapo.

Vitu ambavyo vilirushwa na upepo mkali vinaweza kuwa bado vimebaki kwenye barabara ama pembeni mwa njia za wenda kwa miguu. Watu wanaweza kujikwaa kwenye vitu hivyo, ama kujeruhi miguu yao. Pale unapoendesha, magari yanaweza kugonga mabaki yaliyopo barabarani na kwamba inaweza kupelekea ajali. Na vitu vidogo vinaweza kusababisha pancha.

Shirikisho la Magari nchini Japani ambalo linatoa huduma ya dharura barabarani kwa madereva limesema, pancha imekuwa asilimia kubwa ya matatizo yote. Maafisa wanasema wanaamini visa vingi vinasababishwa na magari kupita kwenye sehemu za paa, kuta ama matawi ambayo yamepeperushwa na kimbunga na kusambaa barabarani kote. Wanasema walipokea simu za dharura 782 katika mkoa wa Osaka pekee katika kipindi cha siku tatu mnamo Septemba mwaka 2018 pale kimbunga kikali kilipolikumba eneo la magharibi mwa Japani.

Hivyo watu wanashauriwa kuendelea kuchukua tahadhari pale wanapoendesha magari baada ya kimbunga kupita, na kuangalia kwa uangalifu hali za barabara.
Taarifa hii inaweza kupatikana kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK. Kama una mwanafamilia ama ndugu katika maeneo husika, tafadhali mtaarifu kuhusiana na taarifa hii.

2. Madhara yanayotokana na pepo kali.

Ifuatayo ni mifano ya madhara yanayoweza kutokea yakisababishwa na pepo za kasi tofauti. Upeo wa papo hapo wa kasimwelekeo ya upepo ya kilomita 144 kwa saa ni mkali zaidi kiasi cha kuangusha mabango na kupindua lori linaloendeshwa.

Upepo wa dhoruba yenye upeo wa kasi ya kilomita 216 kwa saa ni sawa na kasi ya treni ziendazo kasi za Shinkansen. Pepo za kasimwelekeo hiyo zinaweza kuharibu majengo.

Kimbunga kinaweza kuja na pepo za hadi kilomita 288 kwa saa. Miavuli inaweza kuvunja vioo vya madirisha pale inapopeperushwa na pepo kali.

Watu wanashauriwa kuweka mbali vitu ambavyo vinaweza kupeperushwa na pepo kali, kama vile miavuli na nguzo za kuanikia nguo zilizopo nje, kabla ya kimbunga kukaribia na pepo kuongezeka. Vitambaa vilivyoloa na majarida pia vinaweza kuwa hatari pale vinapopeperushwa.

Ni salama kufunga mbao za madirisha nyumbani. Ikiwa nyumba hazina mbao hizo, ni bora kufunika madirisha ya vioo kwa kadibodi ama kuyawekea utando ili kuzuia vioo kuvunjika na kutawanika kutokana na upepo mkali.

Kimbunga kinaweza kusababisha umeme na usambazaji maji kukatika. Watu wanashauriwa kuhifadhi chakula cha angalau siku tatu pamoja na betri.

Ni hatari kuanza maandalizi baada ya pepo za kimbunga kuanza kuvuma. Watu wanashauriwa kujiandaa kabla ya kimbunga kukaribia. Watu pia wanapaswa kuchukua tahadhari ya kutokea kwa dhoruba ikiwa ni pamoja na tonado hata wanapokuwa mbali na kitovu cha kimbunga.

Ikiwa kuna dalili za mawingu ya ghubari, yaani mawingu mazito, kukaribia kama vile radi na kubadilika kwa ghafla kwa pepo ama mbingu kuanza kuwa nyeusi, watu wanashauriwa kutafuta hifadhi katika majengo yaliyo na misingi imara.

Unapokuwa ndani ya jengo, unapaswa kufunga pazia na kwenda kwenye chumba kisichokuwa na madirisha ama kilicho na madirisha machache.

Taarifa hii inaweza kupatikana kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japan.

3. Hatari za maji mengi ya baharini yanayosababishwa na kimbunga.

Na sasa tunakuleta mfululizo wa “Dondoo kuhusu Vimbunga.”
Msimu wa vimbunga umeanza nchini Japani na nchi zingine za Asia Mashariki.
Sehemu yetu ya tatu leo inahusu hatari za maji makubwa ya baharini yanayosababishwa na kimbunga yaani “storm surges” na tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa.

“Storm surges” hutokea wakati kimbunga kinapokaribia au wakati mgandamizo mdogo wa hewa unapojitengeneza, na kunyanyua maji juu ya uso wa bahari. Hali hiyo inayoandamana na pepo kali inasababisha kiasi kikubwa cha maji ya bahari kufurika kwenye maeneo ya fukwe. Hali hiyo mara nyingi imesababisha madhara makubwa sana kote nchini Japani.

Miaka miwili iliyopita kimbunga Jebi kilisababisha “storm surges” katika Ghuba ya Osaka magharibi mwa Japani. Kilisababisha mafuriko katika maeneo mengi ikiwa pamoja na kwenye barabara za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kansai na chini ya ardhi ya jengo la abiria. Urejeaji hali ya kawaida ulichukua siku 17.

Mwaka 2004 kimbunga Chaba kilisababisha “storm surges” katika maeneo mengi ya Bahari ya Seto. Watu watatu walifariki mkoani Kagawa na Okayama.

“Storm surges” inakumbukwa kwa kusababisha madhara makubwa wakati wa kimbunga kilichotokea Ghuba ya Ise mwaka 1959. “storm surges” ilitokea mkoani Aichi na Mie na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 5,000.

“Storm surges” zinapotokea sambamba na mawimbi makubwa, hali inakuwa ya hatari zaidi. Miaka saba iliyopita, 2013, kimbunga Haiyan kilitokea Ufilipino kikiwa na kiini chenye mgandamizo wa hewa wa hektopasko 895. Mawimbi makubwa kwa wakati huo yaliaminika kufikia urefu wa mita zaidi ya 20.

Shuhuda mmoja alisema maji ya uso wa baharini yalikuwa yakiongezeka kwa urefu wa zaidi ya mita 5, ilikuwa “kama tsunami.” Maji hayo yaani “Storm surges” kwa wakati huo ilitokea sambamba na mawimbi makubwa. Hata katika maeneo ambako hali hiyo haikutokea, mawimbi makubwa yalithibitishwa kutokea hadi urefu wa mita 14. Nchini ufilipino watu zaidi ya 7,000 walifariki ama kutojulikana walipo kwa sababu ya kimbunga hicho.

Kujilinda na “Storm surges” kunahitaji uelewa wa hatari zake kwanza. Nchini Japani, maeneo yaliyo hatarini kufurika yanaweza kuangalia ramani za hatari zilizoandaliwa na serikali za maeneo. Kiwango cha mafuriko ya eneo kinachoweza kutokea hutolewa kwa rangi mbalimbali kwenye ramani hizo. Hatari ya madhara yake inakuwa hasa katika kiwango cha juu kwenye “maeneo yaliyo jirani na fukwe au mdomo wa mito” na “maeneo yaliyo usawa au chini ya usawa wa bahari.” Hatua za haraka za kuhama makazi zinapaswa kuchukuliwa mara tu ushauri wa kuhama unapotolewa na serikali za maeneo au onyo linapotolewa juu ya “Storm surges”. Hata hivyo, hali Fulani inapaswa kuzingatiwa. Kimbunga kikiwa karibu, pepo kali huenda zikaanza kuvuma kabla ya mawimbi makubwa kutokea na kufanya iwe vigumu kutoka nje. Ni muhimu kuhama haraka.

4. Kufurika kwa mito.

Mvua kubwa zinazoletwa na vimbunga mara kwa mara zimesababisha mito mikubwa kufurika siku zilizopita. Mwaka 2019, kimbunga Hagibis kilisababisha mto Chikuma katikati ya Japani na mito mingine kuvunja kingo zake katika jumla ya zaidi ya maeneo 140, na kusababisha uharibifu mkubwa katika eneo kubwa.

Hizi hapa baadhi ya hoja tunazopaswa kuzizingatia kuhusiana na kufurika kwa mito kunakoweza kutokea.

Ni muhimu kuangalia mapema ikiwa makazi yako yapo katika eneo lenye hatari ya kukumbwa na mafuriko kwa kutazama ramani ya hatari iliyotayarishwa na mamlaka za maeneo. Pia unashauriwa kuangalia kina kinachokadiriwa cha maji ikiwa makazi yako yatafurika. Ikiwa maji yametabiriwa kuwa na kina cha zaidi ya mita tatu, hii inamaanisha ghorofa ya pili ya jengo inaweza kufurika. Ikiwa yana kina cha zaidi ya mita tano, maji yanaweza kufika ghorofa ya tatu ya jengo.

Nchini Japani, waangalizi wa hali ya hewa wa maeneo wanatoa maonyo ya mafuriko kwa manispaa zinazokabiliwa na hatar kubwa ya kukumbwa na mafuriko. Aidha serikali kuu na za mikoa kwa ushirikiano na maafisa wa hali ya hewa, zinatoa taarifa za hatari ya mafuriko kuhusiana na mifumo mikubwa ya maji. Tahadhari kama hiyo ikitolewa, ni muhimu kuhama makazi yako mapema iwezekanavyo. Hata mto mdogo au mfereji wa umwagiliaji maji inaweza kuwa na hatari kubwa.
Wakati mvua kubwa inapoendelea kunyesha, mto unaweza kufurika na kuvunja kingo zake ghafla. Vifo vingi vilisababishwa wakati watu walikuwa wakisafiri kwa gari au kutembea.

Kwa hivyo, wakati mvua tayari ni kubwa na upepo ni mkali au baada ya kuingia kwa giza, unashauriwa kulinda maisha yako kwa kuhamia ghorofa ya pili ya jengo thabiti badala ya kutafuta hifadhi nje.

Taarifa hii pia inapatikana kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japan.