Taarifa

Bofya linki hapo chini ili kufungua ukurasa maalumu wa maswali na majibu kuhusu virusi vipya vya korona

Orodha ya maswali

1. Virusi vya korona ni nini hasa?
2. Ni kwa njia zipi mtu anaweza akaambukizwa virusi hivyo na kujizuia kuambukizwa?
3. Kina mama wajawazito wanapaswa kujitahadhari na kitu gani?
4. Tunawezaje tukaua virusi kwenye nguo zetu?
5. Ni dalili zipi huonyeshwa na mtu aliyeambukiziwa virusi vipya vya korona?
6. Nani ambaye huonyesha dalili kali ikiwa ataambukizwa virusi vya korona?
7. Watoto wanaweza wakaonyesha dalili kali ikiwa wataambukizwa virusi vipya vya korona?
8. Japani imepata dawa bora ya kuzuia au kutibu maambukizi ya virusi vipya vya korona?
11. Je, ukinawa mikono kwa kutumia sabuni, matokeo ni sawa na yale ya kutumia vitakasa vya kileo?
13. Maambukizi ya virusi vipya vya korona yatasambaa kupitia maji machafu yaliyovuja kutoka kwenye mabomba ya kupitisha maji ya mvua na yale ya maji machafu. Ni kweli?
14. Je, vijana huugua zaidi pale wanapoambukizwa?
15. Je, virusi hivyo hujibadili muundo wake wa jeni?
16. Kwa kiasi gani dawa ya Avigan inafaa katika kutibu virusi vipya vya korona?
19. Je, nitapokeaje yeni 100,000 kutoka kwa serikali ya Japani?”
20. Je, ninaweza kutumia pombe kali kama vitakasa mbadala?
21. Naomba kujua juu ya wagonjwa wa virusi vya korona ambao hawaonyeshi dalili zozote, licha ya kuwa vipimo vinaonyesha kuwa wameambukizwa virusi hivyo.
22. Je, ukoje ufanisi wa barakoa za uso zinazotumiwa mara moja tu, na zile zilizotengenezwa kwa pamba ambazo zinaweza kufuliwa na kuvaliwa tena?
23. Je, tunatakiwa kuzingatia mambo gani pale tunapokuwa ndani ya lifti?
24. Je, natakiwa kufanyaje wakati ambapo wale wanaoishi pamoja kwenye “nyumba ya pamoja ama Share House” wameambukizwa virusi vya korona?
25. Je, ni kwa namna gani tunaweza kuwa makini na kujiepusha na maambukizi ya virusi vya korona kwenye viwanja vya mchezo wa gofu?
27. Je, ni namna gani tunaweza kuwa makini, wakati tunaponunua vitu katika maduka makubwa ya manunuzi?
28. Je, hatari zipi tunakabiliwa nazo tunapokuwa nje tukifanya mazoezi ya kutembea au kukimbia?
29. Ni hatari zipi zinaweza kutokana na hatua ya kuwaruhusu watoto kwenda nje kucheza na wenzao wakati huu wa janga la virusi vya korona?
30. Je, tunapaswa kufanya nini pale tunaposhindwa kuhisi ladha ya chakula?
1: Virusi vya korona ni nini hasa?

Virusi vya korona ni virusi wanavyoambukizwa binadamu na wanyama wengine. Kwa ujumla, virusi hivyo huenea miongoni mwa watu na kusababisha dalili sawa na zile za homa kama vile kukohoa, mafua na kutokwa na makamasi. Aina zingine kama vile Ugonjwa wa Mashariki ya Kati Unaoathiri Mfumo wa Upumuaji, almaarufu MERS uliothibitishwa nchini Saudia mwaka 2012, zinaweza zikasababisha nimonia au dalili zingine hatari.

Virusi vya korona ambavyo vimesababisha janga duniani ni vya aina mpya. Watu walioambukizwa hukumbwa na dalili kama vile mafua, vikohozi, uchovu, kupungukiwa na pumzi, koo zinazowasha na vichwa kuuma. Asilimia ya wagonjwa wapatao 80 hupona baada ya kukumbwa na dalili zisizokuwa hatari. Karibu asilimia 20 hukumbwa na dalili hatari kama vile nimonia au hata viungo vingi vya mwili kushindwa kufanya kazi. Watu walio na zaidi ya umri wa miaka 60, au walio na matatizo mengine kama vile kiwango cha juu cha msukumo wa damu, ugonjwa wa kisukari, ule wa moyo, matatizo ya kupumua au saratani wana uwezekano wa kukumbwa na hali hatari au kufariki. Maambukizi machache yameripotiwa miongoni mwa watoto na dalili zao kwa kiasi fulani si hatari.

2: Ni kwa njia zipi mtu anaweza akaambukizwa virusi hivyo na kujizuia kuambukizwa?

Wataalam wanaamini kuwa virusi vipya vya korona huambukizwa kupitia vitone vya mate au kugusa sehemu iliyo na virusi hivyo kama tu hali inavyokuwa kwa mafua ya msimu au homa. Hii inamaanisha kuwa virusi hivyo huenea kupitia vitone vinavyozalishwa wakati watu walioambukizwa wanapokohoa au kupiga chafya. Mtu pia anaweza akaambukizwa kwa kugusa vitasa vya mlango vilivyo na virusi hivyo, au kanda zinazoning’inia kwenye mabehewa ya treni na kisha kugusa pua au mdomo kwa kutumia mkono uliochafuka. Virusi vya korona vinaaminika kuwa na kiwango sawa cha maambukizi kama mafua ya msimu.

Hatua za msingi za kuzuia maambukizi ya virusi vya korona ni sawa na zile zinazochukuliwa dhidi ya mafua ya msimu. Hizi ni kunawa mikono na kuwa na adabu unapokohoa.

Unaponawa mikono, mtu anashauriwa kutumia sabuni na kuosha kila sehemu ya mikono hadi kwenye kifundo kwa sekunde zisizopungua 20. Au, mtu anaweza akatumia kitakasa mikono chenye kileo. Kuwa na adabu unapokohoa ni njia muhimu ya kudhibiti kuenea kwa maambukizi. Mtu yeyote yule anashauriwa kufunika pua na mdomo kwa kutumia shashi au kiwiko ili kuzuia kuwanyunyizia watu wengine vitone vilivyo na maambukizi. Njia zingine madhubuti ni kuepuka maeneo yaliyosongamana watu, na wakati unaposalia ndani ya nyumba, kufungua madirisha kila wakati ili kuruhusu hewa safi kuingia kwenye nyumba hiyo.

Nchini Japani, kila kampuni ya treni itaamua ikiwa itafungua madirisha ya mabehewa ya abiria yaliyojaa watu. Watalaam wanasema mabehewa hayo tayari yamewekewa hewa safi kwa kiwango fulani kwa sababu milango ya treni hizo itafunguka wakati zinaposimama kituoni na abiria kuingia au kushuka kwenye treni.

3: Kina mama wajawazito wanapaswa kujitahadhari na kitu gani?

Huku kukiwa na mlipuko wa virusi vipya vya korona, Chama cha Wakunga na Wanajikolojia cha Magonjwa Ambukizi nchini Japani kilitoa waraka ukiwashauri kina mama wajawazito na wanawake wanaotazamia kuwa wajawazito.

Chama hicho kinasema hadi kufikia sasa, hakujakuwa na taarifa kuwa kuna uwezekano mkubwa wa wanawake wajawazito kukumbwa na dalili hatari kutokana na virusi vipya vya korona, au kuwepo kwa ripoti za virusi hivyo kusababisha matatizo kwa mtoto ambaye bado hajazaliwa.

Lakini chama hicho kinaonya kuwa kwa ujumla, wanawake wajawazito wanaweza wakawa hatarini ikiwa wataugua nimonia.

Chama hicho kinawashauri wanawake wajawazito kuchukua tahadhari kama vile kunawa mikono ipasavyo kwa kutumia sabuni hasa baada ya kutoka nje na kabla ya maakuli, na kutumia vitakasa mikono vyenye vileo.

Tahadhari zingine zilizopendekezwa zinajumuisha kuepuka kutangamana na watu walio na mafua na wanaokohoa, kuvaa barakoa na kuepuka kugusa pua na mdomo kwa kutumia mikono yako.

Waraka huo ulitayarishwa na Profesa Hayakawa Satoshi wa Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Nihon. Profesa Hayakawa anasema anaelewa wakati kina mama wajawazito wanapokuwa na hofu. Lakini amewataka wanawake kuchukua hatua iliyojikita kwa taarifa sahihi na ya kuaminika kwa sababu aina zote za upotoshaji huenea wakati wa mlipuko wa ugonjwa ambukizi.

4: Je, tunawezaje tukaua virusi kwenye nguo zetu? Tutabaini ikiwa kuosha nguo kunaweza kukaua virusi, na ikiwa tunapaswa kutumia vitakasa vyenye kileo tuoshapo nguo zetu?

Katika kujibu swali hili, Sugawara Erisa kutoka Chama cha Kuzuia na Kudhibiti Maambukizi nchini Japani anasema hakuna haja ya kutumia vitakasa vyenye vileo. Sugawara anaeleza kuwa virusi vingi huoshwa kutoka kwenye nguo zetu kupitia michakato ya kawaida ya uoshaji nguo, ingawa hili bado halijathibitishwa inapokuja kwa suala la virusi vipya vya korona.

Kuhusiana na bidhaa unazohisi zipo hasa kwenye hatari ya kuambukizwa virusi hivyo kama vile hanchifu iliyotumiwa kufunika mdomo unapokohoa au kupiga chafya, Sugawara anapendekeza uviloweshe kwenye maji yanayochemka kwa kati ya dakika 15 hadi 20.

5: Ni dalili zipi huonyeshwa na mtu aliyeambukiziwa virusi vipya vya korona?

Kuna ripoti kuhusiana na suala hili iliyochapishwa na timu ya pamoja ya wataalam ikijumuisha wataalam wa Shirika la Afya Duniani, WHO. Timu hiyo ilifanya tathmini ya kina iliyohusu dalili ya watu 55,924 waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya korona nchini China Februari 20 mwaka huu.

Ripoti hiyo inasema asilimia 87.9 ya wagonjwa walikuwa na homa, asilimia 67.7 walikuwa wanakohoa, asilimia 38.1 walilalamikia uchovu, na asilimia 33.4 walikuwa na kikohozi. Dalili zingine zinajumuisha kupungukiwa na pumzi, koo linalowasha na kichwa kuuma. Wale walioambukizwa walianza kuonyesha dalili katika wastani wa siku 5 hadi 6.

Takriban asilimia 80 ya watu walioambukizwa walikuwa kwa kiasi fulani na dalili zisizokuwa kali. Baadhi hawakupatwa na nimonia. Kati ya watu wote walioambukizwa virusi hivyo, asilimia 13.8 walizidiwa mno na ugonjwa na kutatizika kupumua.

Watu wenye umri wa miaka 60 au zaidi na wale waliokuwa na matatizo mengine ya kiafya kama vile shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa sukari, matatizo ya moyo, magonjwa ya kudumu ya pumzi na saratani walikuwa na uwezekano mkubwa wa kukumbwa na dalili hatari au zinazoweza zikasababisha maafa. Kuna ripoti chache za watoto kuambukiziwa virusi hivyo au kuzidiwa sana na ugonjwa. Ni asilimia 2.4 pekee ya idadi jumla ya walioambukizwa waliokuwa na umri wa miaka 18 kurudi chini.

Daktari Kutsuna Satoshi wa Kituo cha Kitaifa cha Afya Duniani na Tiba amewatibu wagonjwa waliobainika kuambukizwa virusi vipya vya korona nchini Japani. Daktari Kutsuna alisema wagonjwa aliowaona walikuwa wanatiririkwa na makamasi, walikuwa wanawashwa koo na kukohoa. Alisema wote walikuwa wamechoka na homa ya nyuzi 37 au zaidi iliyodumu kwa karibu wiki moja. Kulingana naye, baadhi yao walipatwa na homa kali baada ya wiki moja, na kwamba dalili huonekana kukaa kwa muda kuliko visa vya mafua ya msimu au magonjwa ambukizi ya virusi na mengine.

Taarifa zilizowasilishwa hapa ni za hadi Machi 19.

6: Nani ambaye huonyesha dalili kali ikiwa ataambukizwa virusi vya korona?

Shirika la Afya Duniani, WHO linasema vingi vya vifo vilivyosababishwa na virusi hivyo ni vya watu walio na matatizo ya kiafya yanayodhoofisha mfumo wa kinga mwilini ikiwa ni pamoja na shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa sukari na ule wa moyo.

Ili kuwa na uhakika, watu walio na mfumo dhaifu wa kinga za mwili wanapaswa hasa kuwa wangalifu siyo tu dhidi ya virusi vipya vya korona, lakini pia maambukizi ya kawaida kama vile influenza ya msimu.

Wanajumuisha watu walio na matatizo ya kiafya kama vile shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa sukari, ule wa moyo, wale wanaotumia dawa za ushinikizaji wa kinga ya mwili mathalan ili kutibu rumatizimu na wazee.

Watafiti bado hawajabaini jinsi uhatari wa matatizo ya kiafya ya kudumu ya mgonjwa yanavyohusiana na ukali wa dalili zao.

Inapokuja kwa suala la kina mama wajawazito, hakuna takwimu inayoashiria wako kwenye kategoria iliyo kwenye hali hatari ya kuambukizwa virusi vya korona. Lakini kwa ujumla, huwa wanakabiliwa na uwezekano wa kuambukizwa virusi na ikiwa watapata nimonia, kuna uwezekano mkubwa wa wao kukumbwa na dalili kali.

Hakuna takwimu kuhusiana na ni aina gani ya dalili zinazosababishwa na virusi vya korona kwa watoto wachanga. Lakini ikizingatiwa kuwa hawawezi wakachukua hatua za kujilinda kama vile kunawa mikono na kuepukana na sehemu palikofurika watu, walezi wao wanatakiwa kufanya kila wawezalo kuwalinda watoto hao.

7: Watoto wanaweza wakaonyesha dalili kali ikiwa wataambukizwa virusi vipya vya korona?

Hakuna ripoti yoyote kutoka China kuwa watoto wanaweza wakaonyesha dalili kali ikiwa wataambukizwa virusi vipya vya korona. Tathmini moja iliyofanywa na timu ya wataalam kutoka Kituo cha China cha Udhibiti na Uzuiaji wa Magonjwa iliyohusisha watu 44,672 nchini humo walioambukizwa virusi hivyo kufikia Februari 11 inaonyesha kuwa hakuna mtoto aliye na umri wa miaka 9 au chini ya hapo alifariki kutokana na maambukizi ya virusi hivyo. Ni kifo kimoja tu kilichoripotiwa kati ya wagonjwa walio na umri wa chini ya miaka 20.

Kundi moja la watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Wuhan na taasisi zingine waliripoti kuwa watoto 9 wachanga wenye umri wa kati ya mwezi mmoja na miezi 11 walibainika kuambukizwa virusi hivyo China bara kufikia Februari 6. Wanasema hakuna yeyote aliyezidiwa na ugonjwa.

Profesa Morishima Tsuneo kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Aichi ni mtaalam wa magonjwa ambukizi ya watoto. Profesa Morishima alisema virusi vipya vya korona ni sawia na aina za sasa za virusi vya korona kwa namna fulani na kwamba watoto wanaougua mafua ya kawaida wanaweza wakawa na kiwango fulani cha kinga dhidi ya virusi hivyo.

Hata hivyo Profesa Morishima aliongeza kuwa tunapaswa kuwa na tahadhari kwa sababu maambukizi hayo huonekana kuenea haraka shuleni na kwenye shule za chekechea. Alisema walezi wanapaswa kuhakikisha watoto wananawa mikono yao ipasavyo na kuhakikisha vyumba wanamoishi vina hewa safi.

Taarifa zilizowasilishwa hapa ni za hadi Machi 24.

8: Japani imepata dawa bora ya kuzuia au kutibu maambukizi ya virusi vipya vya korona?

Kwa bahati mbaya, hakuna dawa zilizothibitishwa kuwa bora katika kutibu virusi vipya vya korona kama vile dawa za Tamiflu na Xofluza zinazotumiwa kutibu influenza. Kama tu katika mataifa mengine, madaktari nchini Japani wanaangazia kutibu dalili kama vile kumsaidia mgonjwa kupumua kwa kumuwekea gesi ya oksijeni na dripu za kumuongezea maji.

Ingawa dawa bora ya kutibu virusi hivyo bado haijaendelezwa, madaktari nchini Japani na kote duniani wanawatibu wagonjwa wa virusi hivyo kwa kutumia dawa zilizopo za kutibu magonjwa mengine kwa sababu zinaweza zikatumika kutibu virusi hivyo.

Mojawapo wa dawa kama hiyo ni ile ya Avigan, hii ikiwa dawa ya kutibu mafua iliyotengenezwa na kampuni moja ya kutengeneza dawa ya Japani miaka 6 iliyopita. Mamlaka za China zinasema dawa hiyo ni bora katika kutibu virusi vya korona.

Kituo cha Kitaifa cha Japani cha Afya Duniani na Tiba kinasema kilitumia dawa moja ya kupambana na virusi inayotumika kuzuia kuanza kwa ugonjwa wa UKIMWI kwa mgonjwa mmoja aliyeambukiziwa virusi vya korona. Maafisa wa kituo hicho wanasema homa ya mgonjwa huyo ilipungua, na uchovu na tatizo la kupumua kuimarika.

Juhudi za kutafuta dawa ya kutibu virusi vya korona zinaendelea katika nchi kadhaa. Kundi moja la watafiti kutoka kwenye Kituo cha Marekani cha Udhibiti na Uzuiaji wa Magonjwa limeripoti kutumia dawa ya kupambana na virusi inayoendelezwa ili kutibu ugonjwa wa Ebola, kumtibu mwanamume mmoja aliyeugua nimonia kutokana na virusi vipya vya korona. Watafiti wamesema dalili za mwanamume huyo zilianza kuimarika siku moja baada ya kupewa dawa hiyo. Walisema aliondolewa kwenye mashine ya kumsaidia kupumua kwa kuwekewa gesi ya oksijeni na homa yake kupungua.

Wizara ya Afya nchini Thailand imesema matumizi ya pamoja ya dawa za kutibu mafua na ugonjwa wa UKIMWI ziliboresha hali ya mgonjwa ambaye alipona kutokana na virusi vipya vya korona.

Hata hivyo katika hali zote, wataalam wanasema utafiti zaidi wa kitabibu unahitajika ili kubaini usalama na ubora wa dawa hizo.

Taarifa zilizowasilishwa hapa ni za hadi Machi 25.

11: Je, ukinawa mikono kwa kutumia sabuni, matokeo ni sawa na yale ya kutumia vitakasa vya kileo?

Sakamoto Fumie ni mtaalamu wa udhibiti wa maambukizi kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka jijini Tokyo. Anasema matumizi ya sabuni ni bora kwa kiasi fulani.

Kulingana naye, hii ni kwa sababu sabuni ya kunawia mikono kwa kawaida huwa na kemikali, yaani surfactants zinazoharibu utando wa mafuta unaozingira virusi vya korona. Anasema hii inamaanisha virusi hivyo vinaweza vikaharibiwa kwa kiasi fulani.

Sakamoto anasema vitakasa vya kileo pia ni bora, lakini ikiwa mikono yako ni michafu, wakati mwingine ni vigumu kwa vitakasa hivyo kuingia ndani ya sehemu zilizoambukizwa virusi hivyo.

Sakamoto anawasihi watu kunawa mikono mara kwa mara wakitumia sabuni.
13: Maambukizi ya virusi vipya vya korona yatasambaa kupitia maji machafu yaliyovuja kutoka kwenye mabomba ya kupitisha maji ya mvua na yale ya maji machafu. Ni kweli?

Virusi vipya na vile vya SARS vyote vinatoka katika familia moja ya korona. Virusi vya korona vilivyosababisha SARS vinajulikana kwa kuzaliana mara nyingi si tu kwenye koo na mapafu bali pia kwenye utumbo.

Pale virusi vya SARS vilipoenea miongoni mwa watu kwenye maeneo mengi duniani mnamo mwaka 2003, maambukizi ya watu wengi yaliripotiwa kwenye majengo yaliyo makazi ya watu huko Hong Kong.

Ilishukiwa kuwa maambukizi ya halaiki yalisababishwa na matone ya maji yenye virusi yaliyovuja kutoka kwenye mabomba yaliyozeeka ya kupitisha maji ya mvua na yale ya maji machafu.

Profesa Kaku Mitsuo wa Chuo Kikuu cha Tiba na Dawa cha Tohoku, mtaalam wa hatua za kuzuia maambukizi, anasema kuwa kuna hatari kidogo ya virusi kuenea kupitia mabomba hayo kwenye nchi zenye kiwango cha juu kiasi cha usafi.

Lakini anasema inawezekana kwa virusi kujipandikiza kwenye vyoo na maeneo ya kukizunguka na unaweza kupatwa na maambukizi kwa kugusa maeneo hayo kwa mikono yako.

Alisema watu wanapaswa kufunika mfuniko wa choo kabla ya kumwaga maji ya kusafisha baada ya kujisaidia na kuhakikisha kuwa wamenawa vema mikono yao baada ya kutoka chooni.

Anasema watu wanapaswa kuhakikisha wanadumisha hali ya usafi kwenye maisha yao ya kila siku, kama vile kwa kusafisha koki za maji, sehemu za kunawia mikono na vitasa.

Taarifa zilizowasilishwa hapa ni za hadi Aprili Mosi.

14: Je, vijana huugua zaidi pale wanapoambukizwa?

Wataalam huwa wanasema kuwa wazee na wale wenye magonjwa yanayosumbua kwa muda mrefu huwa na kawaida ya kuonyesha dalili kali zaidi pale wanapoambukizwa virusi hivyo.

Lakini mwezi Machi, 2020, vyombo vya habari viliripoti kwamba mwanamke mwenye umri wa miaka 21 nchini Uingereza na msichana wa miaka 16 huko Ufaransa, waliokuwa hawana magonjwa mengine, walipoteza maisha baada ya kuambukizwa virusi vipya vya korona.

Visa vya hivi karibuni vinaonyesha kwamba baadhi ya vijana wanaweza pia kusumbuliwa sana na maradhi.

Japani pia imeshuhudia visa vya vijana wakiumwa sana. Kutsuna Satoshi wa Kituo cha Kitaifa cha Afya Duniani na Tiba alisema miongoni mwa wagonjwa zaidi ya 30 aliowatibu, mwanaume mwenye umri wa miaka ya mwanzoni ya 40 ambaye hakuwa na ugonjwa mwingine wa muda mrefu alionyesha dalili kali za maradhi hayo.

Kutsuna anasema mwanaume huyo alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya homa na kukohoa tu katika siku kadhaa za mwanzo lakini baada ya juma moja alianza kusumbuliwa sana na homa ya mapafu na alihitaji kifaa cha kumsaidia kupumua kutokana na kuzorota kwa uwezo wake wa kupumua.

Alisema baadaye hali ya mgonjwa huyo iliimarika. Kutsuna alituambiwa kuwa vijana hawapaswi kudhani kwamba hawawezi kuathirika kwani wao pia wanaweza kuumwa sana.

Shirika la Afya Duniani lilionya kuwa kuna visa vingi vya watu wenye umri wa miaka chini ya 50, kulazwa hospitalini.

Kituo cha Marekani cha Udhibiti na Uzuiaji wa Magonjwa kiliripoti kuwa asilimia 2 hadi 4 ya walioambukizwa wenye umri wa kati ya miaka 20 na 44 wapo kwenye chumba cha wagonjwa walio mahututi.

Taarifa zilizowekwa hapa ni za hadi Aprili mbili.

15: Je, virusi hivyo hujibadili muundo wake wa jeni?

Mwanzoni mwa mwezi Machi, kundi la watafiti la nchini China lilitathmini jeni za virusi vya korona kutoka kwa waathirika zaidi ya 100 wa virusi hivyo kutoka kote duniani. Timu hiyo ya watafiti ilibaini tofauti za kijenetiki walizoziweka kwenye aina mbili za virusi vya korona, aina ‘L’ na ‘S’.

Timu hiyo ilibaini kuwa virusi vya aina ya ‘S’ vina muundo wa jeni unaokaribiana kufanana na ule unaopatikana kwenye popo. Virusi aina ‘L’ vilibainika kwa wagonjwa wengi wa kutoka nchi nyingi za Ulaya na vinaaminika kuwa ni aina mpya kulinganisha na vile vya aina ‘S’.

Profesa Ito Masahiro wa Kitengo cha Sayansi ya Uhai cha Chuo Kikuu cha Ritsumeikan anayetafiti juu ya tabia za virusi, anasema virusi vya korona vinabadilika jeni zake kirahisi na vinaaminika kubadilika kupitia kwa watu wengi wanaoambukizwa na kurejelewa kuenea kwa maambukizi ya virusi hivyo.

Katika hatua nyingine, kuhusu uwezekano wa virusi kubadili jeni zake ili kuweza kuwa rahisi kuambukiza, Ito anasema virusi hivyo bado vipo katika hatua ambayo muundo wake wa kijenitiki haujabadilika kwa kiasi kikubwa. Hata kama kuna tofauti ya jeni kati ya aina ‘S’ na ‘L’, bado kuna uhaba wa taarifa juu ya aina ipi ya virusi inayoweza kusababisha dalili kali. Ito anasema wakati ukali wa ugonjwa na viwango vya vifo vikitofautiana miongoni mwa mataifa, inaaminika kutofautiana huko kunasababishwa na watu wenyewe, ikiwemo tofauti ya uwiano wa idadi ya wazee kwenye nchi husika, tamaduni na utamaduni wa chakula.

Taarifa zilizowasilishwa hapa ni za hadi Aprili 3.

16: Kwa kiasi gani dawa ya Avigan inafaa katika kutibu virusi vipya vya korona?

Avigan inayofahamika pia kama Favipiravir, ni dawa ya kutibu influenza iliyotengenezwa na kampuni moja ya kutengeneza dawa nchini Japani miaka sita iliyopita.

Kumekuwa na athari za dawa hiyo zilizoripotiwa kwenye majaribio ya wanyama wa maabara, kwa hivyo serikali ya Japani haijaidhinisha matumizi yake kwa baadhi ya watu kama vile kina mama wajawazito. Dawa hiyo sasa itatumika kuwatibu wagonjwa walioambukizwa virusi vipya vya korona katika visa tu vilivyoidhinishwa na serikali.

Kwa wakati huu, hakuna dawa zingine zinazofahamika zinazofaa kwa matibabu ya wagonjwa wa virusi vipya vya korona, lakini Avigan inatarajiwa kuwa bora katika kutibu virusi hivyo, vinavyozaliana kwa hali sawa na virusi vya influenza. Utafiti juu ya athari za dawa hii unafanyika katika maeneo mengi duniani.

Serikali ya China imetangaza matokeo ya utafiti wa kitabibu uliofanyika kwenye taasisi mbili za tiba. Mojawapo ni iliyopo Mjini Shenhzen kwenye Jimbo la Guangdong ukiwahusisha wagonjwa 80.

Wale ambao hawakutibiwa na dawa ya Avigan walichukua nambari ya katikati ya siku 11 kabla ya matokeo ya majaribio yao kubadilika kutoka kuwa chanya hadi kuwa hasi. Nambari ya katikati ya siku kwa wale waliotibiwa na dawa hiyo ilikuwa nne.

Picha za eksirei zilionyesha kuwa hali ya mapafu ya asilimia 62 ya wagonjwa ambao hawakutibiwa na dawa ya Avigan iliimarika, ilhali asilimia 91 ya wale waliotibiwa na dawa hiyo walipata nafuu.

Serikali ya China imetangaza kwamba matokeo hayo yaliichochea kuijumuisha rasmi dawa ya Avigan kama mojawapo wa dawa za kuwatibu wagonjwa walioambukizwa virusi vipya vya korona.

Nchini Japani, utafiti wa kitabibu unaohusisha wagonjwa 80 wenye dalili zisizokuwa kali ama wale wasioonyesha dalili, umekuwa ukiendelea kwenye taasisi kama vile Chuo Kikuu cha Afya cha Hospitali ya Fujita mkoani Aichi tangu mwezi Machi mwaka huu. Watafiti wanaangazia ni kwa kiasi gani dawa hiyo inaweza ikapunguza wingi wa virusi hivyo.

Kampuni ya Japani inayozalisha dawa ya Avigan imetangaza kwamba imeanzisha majaribio ya kitabibu ili iweze kupata idhini ya serikali. Ikiwa kufaa na usalama wa dawa hiyo vinaweza vikathibitishwa, kampuni hiyo inapanga kutuma ombi la kutaka serikali kuiidhinisha.

Taarifa zilizowasilishwa hapa ni za hadi Aprili 6.

19: Je, nitapokeaje yeni 100,000 kutoka kwa serikali ya Japani?”

Serikali ya Japani imeainisha maelezo ya kina ya mpango wake wa kuwapa wakazi wake wote yeni 100,000 au zaidi ya dola 900 pesa taslimu, kama sehemu ya jibizo lake la kiuchumi kufuatia mlipuko wa virusi vya korona.

Fedha hizo zitatolewa kwa kila mtu aliyeorodheshwa kwenye Rejesta ya Msingi ya Ukaazi ya Japani bila kujali utaifa wao.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Japani Takaichi Sanae aliainisha mpango huo kwenye mkutano na waandishi wa habari Aprili 20 mwaka huu.

Takaichi alisema fedha hizo zitatolewa kwa raia haraka. Maombi na malipo yatafanywa bila watu kukutana ili kuzuia maambukizi na kuwapunguzia makarani kazi kwenye ofisi za manispaa.

Kila mtu aliyeorodheshwa kwenye Rejesta ya Msingi ya Ukaazi ya Japani kufikia Aprili 27 anastahili kupokea fedha hizo.  Hii inamaanisha kwamba mpango huo unajumuisha raia wa Japani pamoja na raia wa kigeni walioorodheshwa kama wakazi na wana viza ya zaidi ya miezi mitatu.

Manispaa zitatuma fomu za maombi kwa wakuu wa kila kaya. Wanaotuma maombi ya fedha hizo watahitajika kupeana nambari ya akaunti yao ya benki, pamoja na nakala za vitambulisho vyao na taarifa za akaunti zao za benki. Fedha hizo kisha zitatumwa kwenye akaunti zao.

Watu pia wanaweza wakatumia mfumo wa kumtambua mtu unaofahamika kama “My Number Card” kutuma maombi ya fedha hizo kupitia mtandaoni.

Kila manispaa inaweza kuamua ni lini itaanza kupokea maombi. Maombi hayo yatakubaliwa katika kipindi cha miezi mitatu.

Manispaa pia zitaamua muda wa kuanza kukabidhi raia fedha hizo. Wizara ya mambo ya ndani inasema huenda baadhi ya manispaa zikaanza kulipa fedha hizo mapema mwezi huu wa Mei.

Watu wanaotaka wasipewe fedha hizo wanapaswa kubainisha hilo kwenye fomu za maombi. Waziri wa Mambo ya Ndani anasema kuwa yeye binafsi hana mpango wa kutuma ombi la kutaka kupewa fedha hizo.

Data zilizowasilishwa kwenye taarifa hii ni za hadi Aprili 22.

20: Je, ninaweza kutumia pombe kali kama vitakasa mbadala?

Wizara ya Afya ya Japani imeamua kuruhusu matumizi ya vinywaji vyenye asilimia kubwa ya kilevi vitumike kama mbadala wa vitakasa, ili kufidia usambazaji mdogo uliosababishwa na janga la virusi vya korona. Uamuzi huo unalenga kujibu wito kutoka kwenye taasisi za tiba na vituo vya makazi maalum kwa wazee ambavyo vimekuwa vikihangaika kuweza kupata vitakasa vilivyotengenezwa kwa kilevi, yaani alcohol-based sanitizers.

Mwezi Aprili, Wizara ya Afya iliviambia vituo hivyo kuwa vinywaji vyenye asilimia kubwa ya kilevi, vilivyotengenezwa na makampuni ya vinywaji vinaweza kutumika kama itakuwa vigumu kupata vitakasa maalum.

Kwa hiyo vinywaji vyenye kilevi cha kati ya asilimia 70 na 83 vinaweza kutumika.  Baadhi ya aina fulani za vodka zipo kwenye kipengele hiki. Maafisa wa Wizara ya Afya pia wanagusia kuwa vinywaji vyenye asilimia zaidi ya hizo vina uwezo mdogo wa kutakasa, kwa hiyo vinapaswa kuchanganywa na maji.

Maafisa wanasisitiza kuwa hiyo ni hatua ya kipekee kwa ajili ya kukabiliana na uhaba wa vitakasa vyenye kilevi, hususan katika vituo vya tiba.

Wanatoa wito kwa umma kuendelea kunawa mikono kwa umakini majumbani ili kuzuia kuenea kwa virusi vya korona.

Data hizi ni za hadi tarehe 27, Aprili mwaka huu.

※Msikilizaji kumbuka kwamba kunywa pombe kali ama vitakasa haikusaidii kuzuia maambukizi ya virusi hivyo bali ni kuhatarisha maisha yako. Idara ya Zimamoto ya Tokyo inatoa tahadhari kuwa vitakasa vya kusafisha mikono vinaweza kuwa chanzo cha moto, basi usitumie karibu na moto kwani inaweza kulipuka na kuleta madhara makubwa.

21: Naomba kujua juu ya wagonjwa wa virusi vya korona ambao hawaonyeshi dalili zozote, licha ya kuwa vipimo vinaonyesha kuwa wameambukizwa virusi hivyo.

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie, kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka jijini Tokyo, anasema kuwa baadhi ya wagonjwa wanaweza wakapona bila ya kuonyesha dalili zozote. Timu ya utafiti nchini China iliripoti kuwa nusu ya wagonjwa waliohojiwa hawakuonyesha dalili kabisa au walikuwa na dalili kidogo.

Lakini Sakamoto anasema tunapaswa kuendelea kufuatilia hali za wagonjwa kwa takribani wiki moja kwa sababu baadhi yao hali zao hubadilika taratibu na wanaweza kuugua kupita kiasi.

22: Je, ukoje ufanisi wa barakoa za uso zinazotumiwa mara moja tu, na zile zilizotengenezwa kwa pamba ambazo zinaweza kufuliwa na kuvaliwa tena?

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie, kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka jijini Tokyo, anasema majaribio mbalimbali yamekuwa yakifanyika juu ya ufanisi wa barakoa katika kukabiliana na virusi vya korona.

Majaribio hayo yanaonyesha kuwa barakoa aina yoyote kati ya hizo mbili ina ufanisi kwa kiasi fulani katika kuzuia matone yasitawanyike pale unapokohoa au kupiga chafya.

Sakamoto anasema hata hivyo, ufanisi wa barakoa yoyote kati ya hizo mbili sio timilifu, na kiwango kidogo cha matone kinaweza kupita na kusambaa.

Kwa hiyo ni vyema kujiepusha kwenda nje pale unapokuwa unakohoa au kupiga chafya.

23: Je, tunatakiwa kuzingatia mambo gani pale tunapokuwa ndani ya lifti?

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie, kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka jijini Tokyo, anasema wengi wetu hatuwezi kupanda ngazi kwenda hadi ghorofa ya 10 au ya 20 kwenye majengo. Tunachoweza kufanya ili kuepuka maambukizi ni kutotumia lifti pamoja na watu wengi, na kuepuka kuongea na watu wengine tunapokuwa ndani ya lifti.

Hatua kama hizo zinaweza kupunguza uwezekano wa kuambukizwa.

Sakamoto anaongeza kuwa ni muhimu kutogusa uso wako kwa kutumia kidole ulichotumia kubonyeza vitufe vya lifti.

Baada ya kushika vitufe hivyo, pia ni muhimu kunawa mikono yako kwa maji na sabuni.

24: Je, natakiwa kufanyaje wakati ambapo wale wanaoishi pamoja kwenye “nyumba ya pamoja ama Share House” wameambukizwa virusi vya korona?

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie, kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka jijini Tokyo, anasema, katika “Share House” kila mtu ana chumba chake binafsi cha kulala, lakini wapangaji wanatumia jiko na choo kwa pamoja. 

Sakamoto anashauri kwamba kitu muhimu cha kufanya ni kuzisafisha sehemu zinazoshikwa mara kwa mara, kama vile mabomba ya maji au swichi za kuwasha taa za umeme kwa kutumia dawa au sabuni zilizozimuliwa, au ikiwa zinapatikana, unaweza ukatumia visafishaji vya kuua viini vya kileo.

25: Je, ni kwa namna gani tunaweza kuwa makini na kujiepusha na maambukizi ya virusi vya korona kwenye viwanja vya mchezo wa gofu?

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie, kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka jijini Tokyo, anasema kwamba baadhi ya watu wanaweza kudhani kuwa mchezo wa gofu hauna athari ya maambukizi kwa sababu ni mchezo unaochezwa nje. Lakini uchezaji wa mchezo huo unaojumuisha idadi kubwa ya watu ni hatari sana.

Viwanja vya mchezo wa gofu vyenyewe vipo wazi nje na havipo kwenye maeneo yaliyofungwa.

Lakini kutumia vyumba vya kubadilishia nguo ama kupata mlo kwenye viwanja hivyo kunakohusisha watu wengi kunafanya hatari ya maambukizi kuwa makubwa.

Kando na hilo, tunapaswa kuwa makini juu ya hatari ya maambukizi baada ya kugusa nyuso zetu kwa mikono bila kujua, ilhali mikono hiyo imegusa maeneo yanayoguswa na watu wengi wasiofahamika.

27: Je, ni namna gani tunaweza kuwa makini, wakati tunaponunua vitu katika maduka makubwa ya manunuzi?

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka ya hapa Japani anasema kuwa tunapaswa kukumbuka kusafisha mikono bila kusahau viganja, ncha za vidole na vifundo vya mikono kwa kutumia vitakasa vilivyowekwa nje kabla ya kuingia ndani ya maduka makubwa ya manunuzi. Anaongeza kuwa, ni vyema kwenda kwenye maduka hayo wakati ambao watu wanakuwa sio wengi.

28: Je, hatari zipi tunakabiliwa nazo tunapokuwa nje tukifanya mazoezi ya kutembea au kukimbia?

Waziri mkuu wa Japani, Abe Shinzo aliusihi umma kujiepusha na shughuli zisizo na umuhimu au zisizo za lazima alipofanya mkutano na wanahabari kutangaza hali ya dharura. Abe pia alisema kuwa sio tatizo kama watu wataenda nje kwa ajili ya mazoezi ya kutembea au kukimbia, jambo ambalo huenda lilitukanganya.

Lakini Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka anasema kuwa hatupaswi kusahau lengo kuu la tangazo hilo, ambalo ni kuwahamasisha watu kujitenga na wengine kwa kiasi fulani. Kama utakimbia wakati unaongea na mtu mwinginge, vijitone vinaweza kusambaa kati ya mtu mmoja na mwingine, jambo ambalo linapaswa kuepukwa.

Lakini ukikimbia nje ukiwa peke yako na hakuna mtu mwingine karibu yako inafaa zaidi kwa sababu hakuna hatari yoyote kubwa inayoweza kutokea.

29: Ni hatari zipi zinaweza kutokana na hatua ya kuwaruhusu watoto kwenda nje kucheza na wenzao wakati huu wa janga la virusi vya korona?

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka ya hapa Japani, anasema kuwa baadhi ya shule za msingi na sekondari za chini za hapa Japani, zimefungua tena viwanja vya michezo ili kuwaruhusu watoto kucheza na wenzao wakati huu ambapo shule zimefungwa kwa muda mrefu kote nchini humo.

Anasema wazazi wengi wanaweza kuwa wanajiuliza iwapo hatua hiyo inaweza kupelekea hatari ya maambukizi, japokuwa wanapenda kuwaona watoto wao wakicheza na marafiki zao ili kupunguza msongo wa mawazo unaosababishwa na kukaa ndani kwa siku nyingi.

Sakamoto anasema inaonekana hakuna matatizo makubwa kwa sasa, kama wazazi watazingatia masuala muhimu kama vile kupunguza kadiri iwezekanavyo idadi ya watoto wanaocheza pamoja, na kuhakikisha michezo hiyo inamalizika ndani ya muda mfupi. Pia wanapaswa kuhakikisha watoto wao wanaosha mikono yao baada ya kurejea nyumbani.

30: Je, tunapaswa kufanya nini pale tunaposhindwa kuhisi ladha ya chakula?

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka ya hapa Japani, anasema takribani asilimia 30 ya wagonjwa wa virusi vya korona, wamekuwa wakisema kuwa walipatwa na dalili za kushindwa kuhisi ladha au harufu ya chakula.

Kama mtu unapatwa na dalili kama hizo, kuna uwezekano wa kuwa umeathiriwa na virusi hivyo. Lakini dalili kama hizo pia zinaweza kutokea pale unapokuwa umeathiriwa na maradhi mengine. Baada ya dalili hizo kuendelea kwa muda fulani, angalia uwezekano wa kuonana na daktari kama utaendelea kupatwa na homa au kupumua kwa shida.