NHK WORLD > Jifunze Kijapani > Mwanzo wa ukurasa wa Kiswahili > Mwalimu Tufundishe > Makundi matatu ya vitenzi (Somo la 40)

Mwalimu Tufundishe

Makundi matatu ya vitenzi (Somo la 40)

Vitenzi vya Kijapani vimegawanyika katika makundi matatu. Kila kundi lina namna yake ya mnyambuliko. “Kundi la kwanza” ni vitenzi ambavyo vina irabu I katika silabi kabla ya MASU. Mfano ni KAKIMASU (kuandika). Vitenzi katika kundi hili vinaponyambulika, silabi kabla tu ya MASU hubadilika.

Ili kuunda umbo la kikamusi la KAKIMASU (kuandika), unabadilisha KI, silabi kabla tu ya MASU, na kuwa KU, kisha useme KAKU. Unapobadilisha kitenzi KAKIMASU kwenye umbo la TA, ambalo linaashiria wakati uliopita au uliokamilika, unabadilisha KI na kuwa I, kisha useme KAITA (niliandika au nimeandika).

Katika somo la 12, ulijifunza mnyamuliko wa umbo la TA kwa wimbo. Tafadhali angalia tena somo hilo.

“Kundi la pili la vitenzi” ni vile ambavyo vina irabu E kwenye silabi kabla ya MASU. Mfano ni TABEMASU (kula). Unapobadilisha kwenye umbo la kikamusi, unabadilisha MASU na kuwa RU, na kusema TABERU. Na unapobadilisha kwenye umbo la TA, unabadilisha MASU na kuwa TA, na kusema TABETA (nimekula). Katika kundi la pili, pia kuna baadhi ya vitenzi vilivyo na irabu I katika silabi kabla tu ya MASU, kama vile MIMASU (kuangalia). Lakini hivi ni baadhi tu ya vitenzi.

Katika kundi la tatu, kuna vitenzi viwili, SHIMASU (kufanya), na KIMASU (kuja). Vinanyambulika katika hali isiyo ya kawaida lakini ni viwili pekee. Kwa hiyo tafadhali kumbuka namna vinavyonyambulika.

Umbo la kikamusi la SHIMASU (kufanya) ni SURU, na umbo lake la TA ni SHITA (nimefanya).

Umbo la kikamusi la KIMASU (kuja) ni KURU. Umbo lake la TA ni KITA (nilikuja).

Unaweza kutembelea tovuti yetu ambapo utaona jedwali linaloonyesha namna ya kunyambua vitenzi katika umbo la TE na katika umbo la NAI pia kwenye nyenzo za kujifunzia.
Hivyo tafadhali angalia jedwali hilo.
*Utatoka kwenye tovuti ya NHK.